Kaunti ya Turkana yazindua chanjo ya mifugo

Turkana imezindua kampeni kubwa ya chanjo na matibabu ya mifugo inayolenga takriban wanyama milioni moja.
Hii inafuatia ongezeko la magonjwa ambayo yameua mifugo katika mwezi uliopita.Zoezi hilo limehusisha kaunti ndogo tano, huku kipaumbele kikipewa maeneo yanayopakana na Uganda na Sudan Kusini, ambapo harakati za kuvuka mipaka zimeongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa.
Naibu Gavana John Erus ameangazia usambazaji wa dawa zenye thamani ya (Sh15 milioni,) kumi na tano akisema uingiliaji kati huo umelenga kupunguza magonjwa ikiwemo Peste des Petits Ruminants (PPR) na trypanosomiasis, ambayo huenezwa na mbung’o.
Mlipuko huu unaleta tishio kwa kaya za wafugaji ambao riziki yao inategemea mifugo kwa ajili ya mapato, chakula na utajiri.Hata hivyo Kaunti hiyo inalenga chanjo, matibabu na vikwazo vya kuhama kwa wanyama ili kudhibiti kuenea na kuzuia hasara zaidi.
Erus amesema kaunti itawatuma maafisa wa mifugo katika maeneo yaliyoathiriwa, ambapo baadhi ya masoko ya mifugo yamefungwa ili kupunguza uhamaji na kupunguza hatari ya maambukizi.Fauka ya hayo Naibu gavana amewasihi wafugaji kuwapeleka wanyama wao kwa chanjo, akisema zoezi hilo litakuwa bure.Afisa mkuu wa maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa samaki Peter Ikaru amesema timu za mifugo zitatumwa katika wodi zilizoathiriwa.
Amepongeza Kurugenzi ya Huduma za Mifugo na Shirika la Chakula na Kilimo, kupitia VSF-Ujerumani, kwa kuunga mkono mwitikio baada ya timu za ufuatiliaji wa kaunti kugundua visa vinavyoongezeka.Hata hivyo Mkurugenzi wa huduma za mifugo kaunti Benson Longo’r amesema kuhama kwa hivi karibuni kwa idadi kubwa ya mifugo kwenda Loima, Lokiriama, Turkana Magharibi, Turkana Kaskazini na Kibish kutafuta malisho kumeongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa.