Wanafunzi 18 na mwalimu mmoja wafariki baada ya paa la shule kuporomoka nchini Pakistani

0
Picha kwa hisani.ya The Star

.

Wanafunzi kumi na wanane na mwalimu mmoja wamefariki dunia baada ya paa la shule kuanguka katika mji wa Peshawar nchini Pakistan, kwa mujibu wa msemaji wa hospitali ya eneo hilo.

Aidha, zaidi ya watoto kumi na wawili wamejeruhiwa katika mkasa huo na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Hata hivyo, baadhi ya majeruhi wamekuwa katika hali mbaya, kulingana na msemaji wa Hospitali ya Lady Reading (LRH), Muhammad Asim, ambaye ameeleza kuwa hospitali hiyo imetangaza hali ya dharura kufuatia tukio hilo.Vilevile, imebainika kuwa watoto waliofariki dunia na kujeruhiwa walikuwa na umri wa chini ya miaka kumi na mitatu.

Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, imesema kuwa mkasa huo wa kuhuzunisha umeishtua taifa zima. Aidha, rais ametoa rambirambi na pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais amewaombea majeruhi kupona haraka na kikamilifu, huku akiziagiza mamlaka husika kuhakikisha kuwa wanapata huduma bora za matibabu.

Fauka ya hayo, amesisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha mkasa huo na kuhakikisha kuwa majengo ya taasisi za elimu yanazingatia viwango vya usalama, ili kuzuia majanga kama hayo siku zijazo.Vilevile, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ameelezea huzuni yake kubwa kufuatia tukio hilo lililotokea katika eneo la Dir Colony, Peshawar.

Sharif amewaombea waliofariki dunia, wakiwemo watoto wasio na hatia, wapate rehema na nafasi njema peponi. Aidha, amezitumia familia zilizofiwa salamu za pole na kuwatakia nguvu na subira katika kipindi hiki kigumu.

Hata hivyo waziri mkuu amewaombea majeruhi kupona haraka na kuziagiza mamlaka kuhakikisha kuwa wanapatiwa huduma zote muhimu za kimatibabu.Kwa upande wake, Gavana wa eneo hilo, Faisal Karim Kundi, ameitaka mamlaka husika kuwasilisha ripoti ya kina kuhusu tukio hilo ili kubaini chanzo chake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *