Marekani yachunguza mashtaka mapya ya mateso dhidi ya Maduro, mkewe

Na Felistars Kahungu
Waendesha mashtaka nchini Marekani wamekuwa wakitarajiwa kuwasilisha mashtaka mapya ya mateso dhidi ya rais wa zamani wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe Cilia Flores, kufuatia madai ya kuwatesa raia wa Marekani waliokuwa wamezuiliwa nchini Venezuela.
Kwa mujibu wa ripoti ya CNN, mashtaka hayo yamehusishwa na madai ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa zaidi ya raia kumi na wawili wa Marekani wakati wa utawala wa Maduro.
Aidha, waendesha mashtaka wamekuwa wakichunguza uwezekano wa kuwafungulia mashtaka watu wengine ambao wamehusishwa na mateso hayo.Hata hivyo, Maduro na Flores tayari wamekuwa wakikabiliwa na mashtaka nchini Marekani yanayohusiana na ulanguzi wa dawa za kulevya na makosa ya kutumia silaha, baada ya kukamatwa nchini Venezuela katika operesheni ya kijeshi ya Marekani mwezi Januari.
Fauka ya hayo, waendesha mashtaka wamekuwa wakimtuhumu Maduro kwa kutumia mamlaka yake ya serikali kulinda na kuwezesha biashara haramu ya dawa za kulevya, huku akidaiwa kushirikiana na magenge ya dawa za kulevya kusafirisha kokeni kwa wingi kuelekea Marekani
.Kwa upande wao, Maduro na Flores wamekuwa wakikanusha mashtaka yote yanayowakabili. Aidha, kesi yao imekuwa ikipangwa kusikilizwa jijini New York mwezi Juni mwaka ujao, huku wawili hao wakiwa wamezuiliwa katika gereza la Brooklyn.
Wakati huo huo, Flores amekuwa akitarajiwa kufika mahakamani kusikilizwa kwa ombi lake la kubadilishiwa masharti ya kifungo kutokana na matatizo ya moyo anayodaiwa kuwa nayo.