Ogeta Afichua Mahali Video ya Raila Akiwa Hospitalini Iliporekodiwa

0
Picha kwa hisani ya The Star

Msaidizi wa zamani wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Maurice Ogeta, amefichua kwamba video iliyosambaa mtandaoni ikimuonyesha Raila akitembea hospitalini baada ya kifo chake, ilirekodiwa Dubai na wala si India kama ilivyodhaniwa.

Akizungumza katika mahojiano na vituo vya televisheni nchini, Ogeta amesema video hiyo ilikuwa ya zamani na ilikuwa imerekodiwa baada ya Raila kufanyiwa upasuaji wake wa kwanza Dubai.

Aidha, Ogeta amekanusha madai yaliyoenea kwamba video hiyo ilirekodiwa nchini India muda mfupi kabla ya kifo cha Raila, akifafanua kwamba kipande hicho kilikuwa cha wakati Raila alipokuwa akipata nafuu baada ya upasuaji wake wa kwanza.

Kulingana na rekodi, Raila alifanyiwa upasuaji mdogo wa uti wa mgongo huko Dubai Juni 21 mwaka wa elfu mbili na ishirini , (2020), katika kituo kinachoendeshwa na shirika la Ujerumani.

Baada ya upasuaji huo, alitumia takriban wiki tatu akipata nafuu kabla ya kurejea nchini Kenya Julai mwaka huo.Hata hivyo, kifo cha Raila kutokana na mshtuko wa moyo Oktoba 15, mwaka uliopita , kilizua maombolezo ya kitaifa huku mipango ya mazishi ikiendelea kwa kasi, kulingana na matakwa yake ya kuzikwa ndani ya saa 72.

Wakati huo huo, video hiyo ilipoibuka mtandaoni, ilichochea hisia tofauti na uvumi kuhusu mazingira ya kifo chake. Fauka ya hayo, nadharia za njama na taarifa zinazokinzana zilienea kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii, yakiwemo Facebook na TikTok, hali iliyowafanya watu wa karibu na Raila kujitokeza kutoa ufafanuzi.Kwa upande wake, dada yake Raila, Ruth Odinga, alifichua kwamba alifanya uamuzi mgumu wa kuzima mashine zilizokuwa zikimsaidia kaka yake kuishi katika hospitali moja nchini India baada ya hali yake kuzorota.

Ruth amesema Raila alikuwa amepumzika katika hoteli moja huko Kerala, India, kabla ya kuhisi uchovu na kuketi chini wakati wa matembezi ya asubuhi. Baadaye, hali yake ilizidi kuwa mbaya na akakimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Aidha, Ruth alisimulia kwamba alisimama kando ya kitanda cha Raila huku madaktari wakithibitisha kwamba hakuna hatua nyingine iliyoweza kuchukuliwa kumwokoa.

Alisema alimshika mkono kaka yake alipokuwa akizima mashine zilizokuwa zikimsaidia kuishi.Vilevile, binti yake Raila, Winnie Odinga, alitetea maelezo yaliyotolewa na familia, akithibitisha kwamba alikuwa chumbani wakati wa matibabu ya mwisho ya baba yake.

Winnie alisema Raila alifariki mikononi mwake kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yamemkabili.Kwa mujibu wa madaktari katika Hospitali ya Devamatha iliyoko Koothattukulam, katika wilaya ya Ernakulam, Kerala, Raila alikuwa akikabiliwa na magonjwa sugu, yakiwemo kisukari, shinikizo la damu, ugonjwa sugu wa figo na historia ya kuganda kwa damu kwenye mishipa ya kina.

Madaktari hao walisema Raila alikuwa amefikishwa hospitalini kwa gari la wagonjwa kutoka kituo cha matibabu ya Ayurvedic alikokuwa akiishi, akiwa hana mapigo ya moyo wala shinikizo la damu lililoweza kutambuliwa. Hatimaye, alitangazwa kuwa amefariki hospitalini asubuhi ya Oktoba 15, 2025.

Kwa upande mwingine, Ogeta, ambaye alikuwa amehudumu kama msaidizi na mlinzi wa kibinafsi wa Raila kwa miaka 29 hadi kifo chake, alisimulia pia matukio yaliyotangulia kuanguka kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *